SAFARI YANGU YA WOKOVU
YESU ASIFIWE SANA...
Nimekuwa nikikutana na jumbe za watu wakitaka niwaeleze niliokokaje? Nikashindwa kumjibu mmoja mmoja badala yake nikawa nikiwaambia nitawajibu siku. Leo ninalitimiza hilo.
Kwa majina naitwa Annah steven Tewele, mwenyeji wa mkoa wa Iringa lakini kwa sasa naishi Dodoma kimasomo. Mama yangu Veronica Sanga aliokoka kitambo sana hata kabla hajaolewa. Enzi za ubinti wake alikuwa mtumishi wa Mungu mzuri hasa kwenye eneo la maombi. Mpaka akatuzaa watoto 4, mimi nikiwa second born, tangu udogo tulikukulia kwenye wokovu wa kurithi kwa mzazi (mama). Tusipoenda kanisani viboko, Hivyo tulikuwa tunakwenda vipindi vya watoto kila jumamosi na jumapili. Nikiwa darasa la tatu nilipata rafiki mle darasani ambaye alikuwa na kundi kama la watoto 5 hivi. Kila siku wanachanga hela (zamani hizo hela za kula shule ni 50 au 100), wakichanga watanunua miwa, vibama, mifudu na visheti kisha tunagawana. Mimi nilikuwa sipewi hela mara chache, hivyo nikienda shuleni bila hela wenzangu watanisema na kunitenga na kuninyima vitu vya kula. Nikaanza kuiba hela nyumbani. Siku ya kwanza niliiba 200 kabatini. ikawa tabia yangu kuiba. Nikiwa darasa la 5 nikawa naiba mpaka 10,000 dukani. Nilikuwa mwizi sana na kanisani naenda. Mpaka namaliza la saba bado nilikuwa naiba nyumbani.
Nikaingia form one pale Iringa girls secondary school. Nikawa mpole tu, siibii watu vitu. Nikiwa form two kwa kuwa walikuwa wanaiba vitu vya wenzao na wananiibia, nikachoka nikaanza kuiba na mimi. Ukiniibia shati na mimi naiba la watu. Ukiniibia soksi na raba na mimi nitaibia watu. Yaani mwendo wa "niibie nikaibe" na nikawa sishikwi. Na kusali nasali fellowship ya PSA (Pentecostal students Association).
Kule Fellowship hata sikuwa na bidii sana. Kwanza kusimama mbele ya watu kuimba ilikuwa ni aibu kwangu. Hata ikifika zamu ya kidato changu kuongoza sifa nilikuwa sitoki mbele najikausha nyuma kabisa kama alivyokuwa anafanya Ireen George Ila nilikuwa nasali kila siku, maombi na mifungo nahudhuria. Nikiwa kidato cha tatu 2017 nilikuwa nasikia mzigo wa kuomba sana na kufunga sana. Nikawa nafanya hivyo. Nikianza kuomba nitaomba kwa machozi, nikianza kuabudu naabudu kwa machozi. Mwaka huohuo 2017 nilibatizwa kwa maji mengi nikiwa shuleni. Tabia za wizi zilipungua kabisa. Tangu hapo nikajikuta naimbaimba kila mara, nikitulia tu mistari inaanza kutiririka kichwani. Nikawa natamani kuimba fellowship ila najiambia nina sauti mbaya sana na aibu nyingi. Siku moja fellowship nilisikia msukumo wa kwenda mbele kuimba wimbo wangu, nikaenda, nikaanza kuimba wimbo unaitwa "MUNGU HATOZI USHURU KWA MAJIBU YA MAOMBI" aiseee watu wakaanza kusimama wanafuatisha, wanashangilia. Nilijisikia vizuri. Mwisho walinipongeza sana. Niliendelea na tabia ya kuimbaimba hasa nikiwa bafuni nitaimba lisaa lizima.
Mpaka namaliza form four, sijawahi kuhubiri fellowship, wala nilikuwa sijui kuhubiri, na ninaaibu kusimama mbele za watu. Kuimba niliimba mara mbili tu nikajikatia tamaa kuwa nina sauti mbaya, sijui kuimba.
Nikaenda advance pale Ibwaga secondary school- Kongwa Dodoma. Nikajiunga na fellowship ya CASFETA . Hapo ndipo nilipohubiri kwa mara yangu ya kwanza kabisa, kale kafeelings sitokasahau na ile amani ya ajabu moyoni nitaikumbuka daima.Tangu hapo nikawa napata ujasiri wa kusimama mbele za watu na kuhubiri. Watu walikuwa wakinielewa sana mpaka wakawa wananiita "Pastor Annah" nikawa napata mialiko kwenda kuhubiri fellowship nyingine kama UKWATA, TYCS na ASSA.nimewahi kufanya pia semina pale shuleni tukiungana fellowship zote za kikristo. Mungu alinipa Neema mno. Nikawa nasoma sana Biblia na kuomba. Siku nyingine nitafunga na kwenda kujificha kwenye pagale la DH nikiomba. Kama kawaida nilikuwa na tabia ya kuimba bafuni kila nilipoingia kuoga. Nikiingia bafuni nitatoka baada la lisaa limoja, wenzangu wananishangaa huwa naogaje? . Hapo nilikuwa naimba nyimbo zangu fellowship na sioni aibu tena. Nikianza kuimba utapenda ninavyocheza Huko shuleni nilikuwa nikiota ndoto za kihuduma mara nyingi, niliota napigana na kundi la wachawi mwisho wakaokoka wote, nimeota nahubiri, naombea. Kuna kipindi shuleni tulikuwa tunasumbuliwa na wachawi, watu wanalipuka mapepo kila siku. Nilikuja kumuota mchawi mwenyewe. Ni hatari.
Siku moja usiku nilipotoka prepo nikalala kitandani nikafumba macho, ghafla nikaona kama nimepelekwa sehemu ina giza jeusi tii nikawa natamani kupiga kelele, midomo haifunguki, nikatamani kufumbua macho nayo hayafumbuki, nikatamani kujitingisha naona nimeganda, nikataabika. Kimoyomoyo nikasema "Namilikiwa na Damu ya Yesu, niachieni" nikaachiwa. Nilipoamka nikawaita Dom zima, nikawaambia kila room mkaombe kwa pamoja kabla ya kulala, kila siku fanyeni hivyo. Watu wakatii, ila baadae walikuja kuuacha huu utaratibu. Hadi nikamaliza form six MUNGU ALIKUWA MWEMA.
Nilipoingia chuo UDOM 2021,Nilishangaa mabadiliko ya kiroho. Wakati watu wanayaacha maadili ya kwao na kuishi maisha ya kichuo na starehe starehe, Mimi niliamua kuwa wa moto. Mabinti wengi wanajioza chuoni, wanajiuza, wanajiachia, wanatoa mimba, nilidhamiria nisiyaishi haya maisha. Sijawahi kuyatamani maisha ya starehe za chuo. Japo haikuwa rahisi ilikuwa ni vita sana. Mawazo yalinishawishi sana ila nilihakikisha ninayashinda. Nikawa napata mzigo wa maombi, nasoma Biblia na machapisho mengine. Nikautumia mtandao wa fb kuhubiria tangu 2021.Mungu hakuacha kunionyesha kule nitakapokwenda miaka ya mbeleni, isitoshe aliwatumia watu wengi kuwaonyesha kule nitakapokwenda mbele. Nilitiwa moyo, nikakaza mshipi. Nikawa naendelea kuota ndoto za kihuduma. Mara nyingine nikiota ndoto kuhusu watu wengine, hazipiti siku nyingi zile ndoto zinatimia kweli.
2023 January, Mungu aliponipa wazo la kuanzisha kanisa la mtandaoni liitwalo HOLLINESS AND RIGHTEOUSNESS MINISTRY,nilikataa nikapuuza kabisa. Nikamwambia mimi mdogo, sijui kitu, siwezi kuongoza na kubeba watu mimi, kwanza sina hao watu... Visingizio vilikuwa vingi lakini msukumo uliendelea kupiga kelele ndani yangu. Nikakumbuka samweli alisumbuliwa na kelele usiku mzima ila alipoitika kelele zilikoma. Nami NIKAITIKA. mpaka sasa tupo tunamtukuza Mungu sana.
Ninasoma na ninafanya huduma. Na ninamuona Mungu sana. Lile litabia la wizi liliyeyuka. Tangu Advance sijawahi iba. Chuoni sijawahi kujihusisha na upuuzi wowote hata kuchezea muda wa mtoto wa watu. Ni mimi na Yesu kwa kwenda mbele.
Ninamshukuru Mungu kwa zawadi na huduma alizoniaminia nikiwa bado Binti,
✍️ Mwinjilisti.
✍️ Mwalimu wa Neno.
✍️ Mwalimu wa mahusiano.
✍️ Huduma kwa mabinti.
✍️Mshauri.
✍️ Mwimbaji.
Mimi ni mtoto wa kiroho wa Askofu Dickson Cornel Kabigumila . Baba yangu huyu ananitambua sana na Neema Niliyo nayo. Katika mikono yake nasonga mbele.
Nimeamua kuwa wa tofauti katika umri wangu huu. INAWEZEKANA ukidhamiria na kuamua. Mazingira ya sasa hayajalishi kabisa. Nina kazi kubwa ambayo bado sijaifanya kabisa. Kwa Neema ya Mungu NITAKWENDA.
MIMI NI UTUKUFU WA MUNGU ULE UJAO.
AKUBARIKI SANA.
***********

AMeN l
ReplyDelete