MAISHA YANAVYONITESA KWA SASA.
“Ni kawaida kwa watu kutafuta hamasa kutoka kwa waliofanikiwa peke yao kwa sababu tunaamini ndio wanaijua njia sahihi ya mafanikio. Binafsi sijafanikiwa kiwango cha kutoa hamasa hiyo kwa wengine lakini nina Imani kuna mtu aliyekata tamaa kabisa atapata nguvu ya kupambana kwa kujua kuwa hayupo peke yake kwenye haya mapambano Mungu ataleta neema yake siku za mbele asilale, karibu jitahidi kusoma ushuhuda wote...”
Yesu asifiwe sana.,
Binafsi niliamini kuwa kila kitu kitakuwa sawa baada ya kumaliza chuo
kwamba nitapata kazi na kila mazuri niliyotamani yatakuja hasa
kuiheshimisha familia yangu lakini hali imekua tofauti kila kukicha
afadhali ya jana, nimetembeza sana vyeti hadi kuomba kazi ikageuka kazi
yenyewe ubaya haina mshahara.
Kila mpango niliojaribu kufanya iwe biashara au wazo lolote hakuna
linapofanikiwa mpaka rafiki zangu wakaanza kuniita Utopianist
(wakimaanisha mtu mwenye mawazo ya ujamaa ambayo hayatekelezeki). Kila
ninachogusa hakiendi ilifika wakati nikashindwa kabisa kulipa koda
mwenye nyumba akanitimua kisiasa nikahamia uswahilini napo hakuna
chochote kilichofanikiwa.
Niliamua kuweka pembeni fahari ya kuwa nimesoma nikaingia site za ujenzi
hakuna chochote pesa haionekani, nimetapeliwa mpaka sikumbuki namdai
nani na nani na ilikuwa kiasi gani.
Baada ya
hapo nikageukia kwenye kufunga scaffold (mabomba ya chuma yanayofungwa
kama jukwaa la kufanyia kazi hasa nje kwenye magorofa) nikazoea umbali
mrefu kuning`inia kama nyani lakini napo sijafanikiwa chochote
nimetapeliwa sana, hadi nikatamani niende kwa mganga niue kabisa
(Nimetubu nina Imani Mungu wangu amenisamehe), Lakini wapi hakuna
chochote hali imekua ngumu nikasamehe nimerudi kuwalamba miguu
walionitapeli mara kibao angalau nipate chochote.
Nilipata kazi ya kufundisha shule za mitaani (education centers)
nikaacha mwenyewe baada ya kuona hakuna ninachopata pesa yote ilikuwa
inaishia kwenye nauli wakati mwingine hata pesa ya kula nilikosa kabisa
plus kuamka saa kumi asubuhi na kulala saa sita kila siku (kwa sababu ya
umbali na wingi wa kazi).
Wakati napambana
angalau angalau maisha yaende msichana wangu akapata mimba na kutokana
na hali yangu akataka kutoa nikamkatalia kabisa nikiamini Mungu ataniona
angalau mtoto azaliwe nitamlea hata kama ni kwa shida sikutaka kuua,
(hii imeleta ugomvi baina yetu nina miezi mitatu sijawahi hata kumuona
nabembeleleza kama namtongoza sasa) bado hajatoa ninaomba Mungu
amuondolee hiyo roho ya kuua.
Mambo hayakaa sawa kodi ya chumba ikaisha sina kitu mwenye nyumba
akataka kunifukuza kweli nilichanganyikiwa kuna wakati natembea machozi
yanatoka yenyewe najizuia kulia hadharani hapa ndipo kiu ya bangi na
sigara ilipokuja juu angalau usiku niweze kulala na kuamka na nguvu
(nashukuru Mungu amenisaidia nimeacha vyote), kitu pekee ninachoendelea
kuamini ni kwamba Mungu hana ubaguzi kila mtu ana zamu yake, ya kwangu
itafika nijitahidi niendelee kua hai.
Baada ya kukwama sana niliamua kujilipua na kwenda ferry kutafuta kazi
za uvuvi nikiwa sijui chochote wala simjui yeyote nilichohitaji ni
kupata pesa ya halali, ukweli hata kuogelea sijui na sijawahi kupanda
chombo chochote cha majini Zaidi ya pantone. Mungu alisaidia nikapata
nafasi nikakesha baharini siku mbili mfululizo (sikupata hata mia ya
faida Zaidi ya samaki wadogo sita nilirudi nikala na ugali).
Baada
ya hapo nikakosa hata nauli ya kwenda ferry kufanya kazi nitaanza
kwenda tena Mungu akijalia uzima.
Nakumbuka sikumwambia mtu yeyote kua naenda kuvua samaki nilichofanya
nilichukua kitambulisho changu nikakifunga kwenye nguo ili lolote
likitokea watu wanitambue baadae hofu ikazidi nikamwambia dada yangu kwa
sharti la kutosema kwa yeyote Mungu ananitunza kila leo kesho itakua
njema.
Wakuu siongopi kuna wakati zinakata hadi wiki mbili chakula changu ni
ugali mboga ni uji wa chumvi mambo yakikaa sawa ni uji sukari angalau
nikiwa site ndio nakula kawaida sitaki kila mtu ajue tabu yangu.
Nashukuru Mungu ameweka tabasamu kwenye uso wangu kila wakati si rahisi
kujua hadi nikwambie. Mama yangu amekua mgonjwa kwa kazi ngumu hadi
alilazwa nilichoweza kusaidia ni kulia tu nilikosa hata mia ya kumtumia,
anajikaza anatoka kufanya kazi Mungu mwema anamtunza siku moja apate
nafsi ya kula jasho langu ndicho ninachoomba kila siku.
Kuna
wakati nawaza kuhusu mwanangu aliyeko tumboni ambaye sijui kama mama
yake atabadilisha mawazo au vipi maumivu yanazidi najihisi kuhumiwa sana
moyoni nitakuwa baba gani iwapo hiyo mimba ikitolewa ninayeruhusu
mwanangu afe kwa sababu nimeshindwa kumudu maisha lakini kesho itafika
Mungu ataachilia neema naendelea kuomba tu (kufunga siwezi vidonda vya
tumbo vitaniua). Nikiongeza madeni niliyoshindwa kulipa nazidi kuchoka,
niuze laptop yangu iliyochoka ambayo sitapata hata laki moja na
haitamaliza shida akili inagoma au niifanye mtaji wa biashara naogopa
nayo itakufa kama nyingine zilizopita kikubwa uzima tu.
Nikifikiria kurudi nyumbani mkoani hali ni ngumu nachanganyikiwa kabisa
ni bora niwe mbali nisiione hiyo hali nilijiapiza kufa nikitafuta pesa
ya halali siwezi kufanya hila.
Mtafutaji
mwenzangu usichoke jipe moyo kazana Mungu hajatutupa wakati wetu utafika
usiwaze kutajirika kwa dhuluma afya ndiyo zawadi kubwa kuliko zote
Mungu aliyotupa, omba pambana Mungu atasaidia hakuna utajiri wenye Amani
kama hautoki kwa Mungu na kama huwezi kuutumia kusaidia ndugu na jamii
inayokuzunguka. Kwenye Biblia (nimesahau ilipoandikwa) Yesu alimwambia
mtume Petro kuwa kuna wakati shetani atampepeta kama ngano lakini
amemuombea ili Imani yake isiyumbishwe atakapokuwa imara awaimarishe
wengine.
Kuna siku Mungu atafungua malango ya
mbingu mvua itatunyeshea jiitahidi usije ukasahau kuwasadia wahitaji
ndio njia pekee ya kurudisha shukrani kwa Mungu.
Inuka songa mbele kesho hatuifahamu kazi yako ni kuamini kuwa Mungu
anakuwazia mema siku zote hawezi kukuacha hajakusahau anakujua wewe ni
wa kwake na atakupa kwa wakati wake kuwa na uvumilivu.
Jitahidi sana kutunza Amani ya moyo wako na hakika utafanikiwa.
####################
JE, UNA USHUHUDA AMBAO UNGEPENDA TUUCHAPISHE??
Fanya hivyo ili maelfu wajue mambo ambayo MUNGU alikutendea na kupitia ushuhuda wako maelfu ya wasomaji watayashuhudia matendo ya Mungu uliyenaye.
Endapo unao Ushuhuda tafadhali BOFYA HAPA
Mungu Ni mkuu Sana
ReplyDelete