NILIWAZA KUJIUA NILIPOKUWA NA MIAKA 13 TU

 


Jina langu ni Sanjo Mlimba, mwenyeji  wa Kisesa, Mwanza. Hadithi yangu ilianza zamani sana kabla sijaathirika na uraibu wa madawa . Nakumbuka Nilikuwa na umri wa miaka 13 tu nilipowaza kwa mara ya kwanza kujiua.

Sikuelewa ule upweke niliokuwa nao kipindi hicho ulitokana na nini .Nilikuwa sipendi kabisa kuchangamana na watu kabisa. sikuwa na marafiki , hata nikiwa nyumbani nilikuwa napenda kukaa mwenyewe chumbani. Nikiwa shule, kuna wakati naweza kutoka tu darasani nikaenda kukaa kichakani mwenyewe.  lakini sasa naona kwamba adui alikuwa  anajaribu kuikatisha stori yangu kabla hata haijaanza vizuri. Kuna wakati nilikuwa naona kuishi duniani hakuna maana yoyote. Naona tunaenda shule kila siku, mara watu wanaenda mjini wanarudi ,watu wanaenda ziwani kuvua mara shamba hayo yote kwangu nilikuwa naona hayana maana kabisa .Sijui nilikuwa na pepo gani ila ni kwamba nilikuwa sion maana yoyote ya kuishi.

Siku moja nikiwa darasa la sita , niliamka mapema kwenda shule kama kawaida. Mama alikuwa bado hajaamka. nilichukua shilingi mia tano kwenye pochi yake (maana alikuwa akiuza vitumbua) . ilipofika mchana wakat wa mapumziko, nilibeba mfuko wangu wa madaftari maana sikuwa na mpango wa kurudi darasani milele. Nilichukua ile shiling 500 nikenda kununua sumu ya panya kwa wale machinga wanaotembeza mtaani. niliitia mfukoni nikisubiri pumziko iishe wanafunz warudi madarasani. BAADA ya hapo nilikwenda kwenye kichaka kilekile nilichopenda kujificha. Nilikaa kwenye gogo ambalo nakaa siku zote. Niliichukua ile pakti ya sumu ya panya na kuishikilia mikononi huyu nikihisi uzito wa kichwa ukiongezeka. Niliinamisha kichwa kisha nikapata hisia ya kulia. Na kweli nikaanza kulia japo kimya kimya. Niliendelea kulia na kila nilipojaribu kunyamaza ili nifanye nilichopanga kufanya, nilijikuta naangua kilio zaidi . Nikiwa katikati ya machozi, nilihisi mtu akinigusa begani nyuma yangu. Kwa mshituko, nikakuta ni mzee Songe aliyekuwa akipita njia jirani na kichaka hicho. "Mwanangu, unadhani uko sahihi" alinihoji nikiwa sina majibu. Aliinua akanipeleka nyumbani.

Nilivyoendelea kukua, nilijaribu kuziba ule upweke uliokuwa ukinikubwa hata kwa kujaribu kuweka concenntation kwenye mambo mengine hasa  uvuvi kumsaidia babu. 

Baada ya kuhangaika na hali hiyo, nilishauriwa nitumie bangi na kweli kuna kias nilihisi uchangamfu ulionilazimisha kuchangamana na watu. Baada ya kuzoea, addiction hiyo ndo ikawa njia ya kuinusuru nafsi yangu dhidi ya jambo hili na mengineyo niliyoshindwa kukabiliana nayo. 

Nilidhani nilikuwa nimepata udhibiti wa maisha yangu, lakini kumbe nilikuwa nimepotea kabisa.

Nilipotimiza miaka 21, kila kitu kilikuwa tete. Nilizidisha kiwango cha unga (overdose) kiasi kwamba nilikuwa nazimia hata kwa masaa kadhaa. Pamoja na hayo, Mungu hakunitupa.

Hakuna njia nyingine ya kueleza jambo hili. Haikuwa bahati, ila ilikuwa ni intervention ya  kimungu.

Lakini hata baada ya hapo, bado sikumgeukia Yeye. Nilirudi kwenye mambo yale yale  na kujaribu kila siku  kuyakimbia maumivu yale yale.

Siku moja nilikwenda Maeneo ya Sumve barabara ya Musoma, tukakutwa na ajali ya mbaya ya gari, tukio lingine ambalo lingeweza kuukatisha uhai wangu. Bado, nilitoka nikiwa mzima.

Mungu aliendelea kunong'ona ndani yangu, "Bado niko hapa," lakini sikuwa tayari kuisikiliza. Ilinichukua miaka kadhaa kuona jinsi Mungu alivyokuwa akinirejesha kila nilipokuwa katika hatari ya kuangamia. Kila wakati nilipopaswa kufa, Yeye alinilinda niwe hai. Kila mara nilipokata tamaa, Alipuliza tena pumzi ya uzima ndani yangu.

Kisha ikafika tarehe 3 Juni 2025, siku ambayo sitaisahau. Nilijikuta kwenye giza tena, nikiwa nimeshikwa na ile hari ya kutotaka kabisa kuishi, nikiwa katika hali hiyo, nilikuwa sioni maana yoyote ya kuwepo duniani. Lakini katika wakati uleule, dada yangu aliyeko mbali (Dodoma) alinitumia SMS ambayo ni kama ilinihuisha moyo, ilitokea tu maana sikuwa nimewasiliana naye kwa kama miezi miwili. Ujumbe wake ulikuja kwa wakati muafaka kabisa, na nilijua haikuwa yeye tu—alikuwa ni Mungu akizungumza kupitia yeye, akinikumbusha kwamba ushuhuda  wangu haikukusudiwa uishie  kwenye masikitiko.

Ujumbe ule ulivunja uongo uliokuwa unaniambia kwamba sikuwa na thamani ya kuokoka. Kesho yake ilikuwa siku ya ijumaa, ambapo katika mtaa ule kuna kanisa ambalo ibada zikiwa zinaendelea huwa naskia maana sio mbali kutoka kwetu. Nikiwa nimebeba mzigo mzito moyoni nilikokota kwenda kwenye kanisa lile bila kujua naenda kuwaambia nini pale kanisani . Nilipofika walikuwepo watu wachache ambao ni kama walikuwa wanajua kilichokuwa kimenipeleka. Naam, kuyakabidhi maisha yangu kwa YESU.

Tangu jioni ile, nilipata uponyaji wa nafsi yangu. Nilianza kuona neema na kila nira zilizokuwa zikiendesha  maisha yangu zikikatika: 

Hakuna kitu kilichopotea bure. Kila kitu kilikuwa na kusudi.

Mungu aligeuza maumivu yangu kuwa kusudi, udhaifu wangu kuwa ushuhuda, na aibu yangu kuwa nguvu. Alinionyesha kwamba hata katika uasi wangu, Hakuwahi kuniacha.Kila mara nilipokaribia kufa, Alikuwa akinipigania.Leo hii, niko hai si kwa sababu nilistahili nafasi nyingine, bali ni kwa sababu Mungu alinipa nafasi hiyo.

Kama uko katika sehemu hiyo ambayo huwezi kuona mwanga—ng'ang'ana, usikate tamaa. Hata wakati huwezi kumhisi, Bado yupo hapo. Nimejifunza mimi mwenyewe kwamba Mungu haondoki kamwe, na neema Yake haiishi.

Utukufu wote ni kwa Yesu Kristo—Mwokozi wangu, sababu yangu ya kuishi, na nafasi yangu ya pili.

UBARIKIWE

####################

JE, UNA STORY/USHUHUDA AMBAO UNGEPENDA TUUCHAPISHE?? 
 Endapo unao Ushuhuda tafadhali BOFYA HAPA

Comments

Popular posts from this blog

NILIVYOTOKA KUWA MUIMBA KWAYA HADI KUJIUZA NA KUKUTANA NA YESU TENA

JINSI NILIVYOTAHADHARISHWA KABLA YA AJALI

SAFARI YANGU YA WOKOVU